Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Mbeya umefungua njia 106 za pembezoni mwa mradi wa ujenzi wa barabara ya njia nne kutoka Nsalaga hadi Ifisi, hatua inayolenga kupunguza usumbufu kwa wananchi na wafanyabiashara wakati ujenzi ukiendelea.
Hatua hiyo ni utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, wakati wa ziara yake ya kikazi jijini Mbeya, Oktoba 16 na 17 mwaka huu.
Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mbeya, Mhandisi Suleiman Bishanga, amesema mkandarasi ameagizwa kuongeza kasi ya ujenzi kwa kufanya kazi usiku na mchana ili mradi ukamilike kwa wakati. Amesema tayari kazi ya kumwaga lami imeanza katika sehemu ya kilomita tatu zilizopo ndani ya Jiji la Mbeya.
Mradi huo wenye thamani ya shilingi bilioni 138 unahusisha ujenzi wa barabara ya njia nne yenye urefu wa kilomita 29, kuanzia Nsalaga eneo la Uyole hadi Ifisi karibu na Kiwanja cha Ndege cha Songwe.
Baadhi ya wananchi wameeleza kufurahishwa na kufunguliwa kwa njia hizo, wakisema kumepunguza changamoto walizokuwa wakikabiliana nazo wakati wa ujenzi.
Salim Ngaola, dereva wa lori anayesafirisha mizigo kutoka Dar es Salaam kwenda Congo, amesema upatikanaji wa njia za kupita ni muhimu kwa madereva wanaosafirisha mizigo masafa marefu.
Post a Comment