Uongozi wa shule ya Madalaqu Islamic English Medium School, kupitia kituo chake cha malezi na elimu ya awali cha Madalaqu Day Care Centre kilichopo Mbagala jijini Dar es Salaam, umefanya sherehe ya mahafali ya kuwapongeza na kuwaaga wanafunzi wanaohitimu elimu ya awali na kujiandaa kuingia darasa la kwanza.
Mahafali hiyo yamehudhuriwa na wazazi, walezi, walimu, pamoja na wageni mbalimbali waalikwa waliojumuika kushuhudia vipaji na maendeleo ya kitaaluma na kimaadili ya watoto hao.
Akizungumza katika mahafali hayo, Afisa Ustawi wa Jamii Kata ya Mbagala Kibonde Maji, Badru Luyaya, amesema ataendelea kutoa ushirikiano wa karibu na kituo hicho katika masula ya malezi ili kuendelea kujenga taifa na maendeleo kwa ujumla.
Aidha, ameupongeza sana uongozi wa Madalaqu, walimu na wafanyakazi wote wa Madalaqu kwa kufanya juhudi na jitihada za kuhakikisha watoto wanapata elimu bora inayozingatia malezi bora.
Kwa upande wa Mkurugenzi wa Shule za Madalaqu, Sheikh Hussein Ally Bakari, amesema kuwa dhamira kuu ya kuanzishwa kwa vituo na shule zote zilizo chini ya Al Madrasatul Madalaqu ni kuhakikisha mtoto anapata elimu bora inayofuata mtaala wa Serikali na inayoenda sambamba na maadili ya dini ya Kiislamu.
Amesema shule hizo zinaendeshwa kwa mtaala wa kiserikali, lakini pia zinajikita zaidi kwenye masuala ya dini ya Kiislamu ambapo mtoto anapomaliza elimu ya awali anakuwa amemaliza juzuu ya Amma.
“Na tunamwendeleza mtoto huyu, anaingia shule ya msingi, na akifika shule ya msingi mpaka akimaliza darasa la saba, mtoto huyu huwa amemaliza msahafu mzima kwa kusoma, lakini pia kwa kuhifadhi ni juzuu 15.
“Kwa hiyo, tunafanya hayo pamoja na malezi ya watoto wetu kimaadili, kinidhamu na kimpangilio ambapo mtoto anapata taratibu zote za kisheria pamoja na za kimila. Lakini pia, tunaendesha mambo yetu haya kwa uadilifu wa hali ya juu ikiwemo kuwasimamia watoto hawa zaidi kwa ajili ya maadili ili kujikinga na mmomonyoko uliopo,” amesema Sheikh Husein.
“Na watoto wetu wanajifunza katika lugha mbili hususan lugha ya kwanza ni lugha ya Kiingereza, lugha ya pili ni lugha ya Kiarabu. Na lugha ya tatu huwa tunazungumza Kiswahili kwa sababu sote sisi ni Waswahili. Kwa hiyo, hizo lugha zinapatikana katika shule zetu,” amefahamisha.
Katika hatua nyingine, ametoa rai kwa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kutumia fursa hiyo ya kuwapeleka watoto katika shule za Madalaqu ambazo ni Madalaqu Pre and Primary School iliyoko Mwanambaya kuanzia elimu ya awali mpaka darasa la saba, pamoja na JB Islamic Pre and Primary School iliyoko Chamazi Kwa Mzara, huku akieleza kuwa ada zao ni nafuu na zinalipwa kwa awamu.
“Kwa upande wa vituo vya kulelea watoto wadogo, kuna Madalaqu Day Care Centre iliyoko Mbagala Rangi Tatu na Madalaqu Day Care Centre iliyoko Chamazi mtaa wa Kwa Sungura. Kwa hiyo, tunaomba mwalete watoto katika shule zetu ili waweze kupata maadili mema ya dini yao na dunia yao,” amesisitiza Sheikh Husein.
Aidha, amesema wanajivunia kuwa malengo ambayo wameyaweka pale mtoto anapofika darasa la saba awe amemaliza juzuu 30 yametimia kwa asilimia kubwa.
Kutimizwa kwa malengo hayo kunachangiwa na kuwepo kwa kitengo cha madrasa kinachowasaidia wanafunzi kupata malezi bora ya kiimani ya dini ya Kiislamu.
Kwa upande wake, Msimamizi katika upande wa dini, Ustadh Mabrouk Hussein, amesisitiza umuhimu wa malezi ya kiroho na maadili ya Kiislamu katika makuzi ya mtoto, akibainisha kuwa elimu ya dunia pekee bila msingi wa dini haiwezi kumjenga mtoto kuwa raia mwema.
Kwa upande wao, baadhi ya wazazi waliohudhuria mahafali hayo walipongeza juhudi kubwa zinazofanywa na walimu pamoja na uongozi wa taasisi ya Al Madrasatul Madalaqu kwa mabadiliko chanya wanayoyaona kwa watoto wao, hususan katika nidhamu, kujiamini, na uelewa wa masomo.
Aidha, hafla hiyo ilipambwa na uwepo wa wakuu wa shule zilizo chini ya mwavuli wa taasisi ya Al Madrasatul Madalaqu, wakiwemo Mkuu wa Shule ya Madalaqu Islamic English Medium School Mwanambaya (Mkuranga), Mkuu wa Shule ya Madalaqu Day Care Centre Chamazi Magengeni, Mkuu wa Shule ya JB Islamic, pamoja na mwenyeji wao, Mkuu wa Shule ya Madalaqu Day Care Centre – Mbagala.
Katika mahafali hayo, wanafunzi walipata fursa ya kuonesha umahiri wao katika nyanja mbalimbali ikiwemo kusoma kwa lugha ya Kiingereza, kuhifadhi na kusoma Qur'an Tukufu, nyimbo, ngonjera, pamoja na michezo mbalimbali iliyodhihirisha msingi imara wanaoupata kituoni hapo.
![]() |
| Baadhi ya Walimu wa Shule za Madalaqu |
![]() |
| Mkurugenzi wa Shule za Madalaqu, Sheikh Hussein Ally Bakari |









Post a Comment